Serikali imeanza kuchimba visima virefu katika vijiji vya Jitulola na Masinono, vilivyopo kata ya Bugwema, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, mkoani Mara. Mradi huu unalenga kuchimba visima viwili virefu ili kuwasaidia wakazi takriban 15,000 katika vijiji hivyo, ambao wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji safi kwa muda mrefu.
Wananchi wa vijiji hivi wameonyesha furaha yao kwa serikali, wakisema kwamba mradi huu umewaletea matumaini mapya. Kwa miaka mingi, wamekuwa wakilazimika kugawana maji na mifugo, hali iliyosababisha ugumu wa maisha. “Tunaishukuru serikali kwa hatua hii. Mradi huu umekuja wakati muafaka na hakika utapunguza adha kubwa tuliyokuwa tukikabiliana nayo,” alisema Mwamvua Josephat, mmoja wa wakazi wa Jitulola.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Musoma, Mhandisi Edward Sironga, alibainisha kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha upatikanaji wa maji safi kwa wakazi wa maeneo yaliyo na changamoto. Alisema kuwa mradi huo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kwamba visima vingine vitatu vitachimbwa katika maeneo tofauti ya halmashauri hiyo.
Serikali ina matumaini kuwa mradi huu utaleta suluhisho la kudumu kwa changamoto ya maji safi, na hivyo kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa vijiji hivyo.
#KonceptTvUpdates