Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imepokea dozi 50,000 za chanjo ya Mpox kutoka Marekani, ikiwa ni wiki moja baada ya shehena ya kwanza ya chanjo kutoka Umoja wa Ulaya kuwasili nchini humo. Cris Kacita Osako, Mratibu wa Kamati ya Kukabiliana na Mpox, amesema mpango wa utoaji chanjo utaanza rasmi Oktoba 2, 2024, katika majimbo yaliyoathirika zaidi na mlipuko huo.
Hii inakuja baada ya ripoti za hivi karibuni kufichua changamoto kubwa zinazowakabili wahudumu wa afya nchini humo, hasa katika maeneo kama Kivu Kusini, ambako ugonjwa wa Mpox umeenea kwa kasi. Wahudumu wa afya katika eneo hilo wamelalamikia ucheleweshaji wa chanjo huku idadi ya wagonjwa wengi wao wakiwa watoto wachanga, ikiongezeka kila siku.
Ikumbukwe, Mpox, ambao ni ugonjwa unaoambukiza kwa urahisi, umesababisha vifo vya watu 635 mwaka huu pekee nchini DR Congo. Japokuwa chanjo zinaonekana kuwa suluhisho muhimu katika kudhibiti ugonjwa huo, changamoto ya upatikanaji na usambazaji imekuwa kubwa, hasa katika maeneo yenye maambukizi makubwa kama Kivu Kusini. Hata baada ya kuwasili kwa chanjo 200,000 kutoka Umoja wa Ulaya, usambazaji wake bado unasuasua.
#KonceptTvUpdates