Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA-Bara, Tundu Lissu, ametoa wito kwa serikali kuanzisha uchunguzi wa kimataifa kuhusu matukio ya uhalifu, ikiwemo utekaji na mauaji yanayoripotiwa nchini. Akizungumza katika mahojiano na *JamboTV*, Lissu alieleza kuwa Vyombo vya Usalama nchini haviwezi kuchunguza matukio hayo kwa sababu vinatuhumiwa kuhusika moja kwa moja.
“Lini Jeshi la Polisi liliwahi kuchunguza chochote kuhusu haya mambo? Hatuezi kusema Vyombo vya Usalama vichunguze utekaji au mauaji wakati vinavyohusika ni hivyo hivyo. Vinahitaji kuchunguzwa na kusafishwa ili kuhakikisha hakuna majambazi walio katika sare za majeshi na kulipwa na serikali,” alisema Lissu.
Katika mahojiano hayo, Lissu aliongeza kuwa njia ya kawaida ya kuchunguza matukio makubwa ya uhalifu ni kupitia Tume ya Kijaji ya Uchunguzi. Hata hivyo, alieleza wasiwasi wake kuwa mfumo huo nchini Tanzania sio wa kuaminika kwa sababu tume hizo huwasilisha ripoti zake moja kwa moja kwa Rais.
“Tume ya Kijaji hapa Tanzania inaripoti kwa Rais, na hiyo si njia sahihi ya kupata haki. Njia pekee ya kuhakikisha uchunguzi wa haki ni kwa kuanzisha uchunguzi wa kimataifa unaoendeshwa na wataalamu huru kutoka nje ya nchi,” alisisitiza.
Matukio ya utekaji na mauaji nchini yameibua mjadala mkali miongoni mwa wananchi na wanasiasa, huku baadhi ya watu wakidai kuwa vyombo vya dola vinahusika moja kwa moja na uhalifu huo. Wito wa Lissu wa kufanywa uchunguzi wa kimataifa umeibua maswali mapya kuhusu uwajibikaji wa vyombo vya usalama nchini na utayari wa serikali kukabiliana na tuhuma hizo.
#KonceptTvUpdates