Mkazi wa Mtaa wa Sulungai, Kata ya Ipagala jijini Dodoma, Elizabeth Sudai (80), ameomba msaada kutoka serikalini ili kurudishiwa nyumba yake, ambayo imeuzwa kinyemela na mjukuu wake baada ya kuiba hati na nyaraka muhimu za mali hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Elizabeth alieleza kuwa tukio hilo lilitokea mwaka jana wakati alipokuwa safarini kuuguza mgonjwa kijijini kwao. Aliporudi, aligundua kuwa mjukuu wake alikuwa ameiuza nyumba hiyo kwa Shilingi milioni tano kwa mtu anayedaiwa kuwa mtumishi wa serikali.
“Nikiwa safarini, mjukuu wangu aliiba hati ya nyumba na nyaraka nyingine, kisha akauza nyumba bila ridhaa yangu. Niliporudi nikakuta nyumba yangu imeuzwa,” alisema Elizabeth kwa uchungu.
Baada ya kugundua uuzaji huo, Elizabeth alikwenda polisi na kufungua kesi, ambapo mjukuu wake na mnunuzi walikamatwa. Polisi walibaini kuwa mjukuu ndiye aliyekuwa na makosa, na kutokana na hali hiyo, walikubaliana kufanya makubaliano mapya na mnunuzi, ambapo nyumba ilipaswa kuuzwa kwa Shilingi milioni 45.
“Mnunuzi alipaswa kulipa kiasi kingine kilichobaki, lakini hadi sasa ameweza kulipa Shilingi milioni 10 pekee, huku salio likiwa halijalipwa,” alifafanua Elizabeth, akiendelea kuomba msaada wa serikali ili kupata haki yake.
Tukio hili linaibua maswali kuhusu usalama wa wazee na mali zao, huku Elizabeth akiwa mfano hai wa changamoto zinazowakabili wazee wanapokutana na udanganyifu kutoka kwa watu wa karibu, ikiwemo familia. Serikali imeombwa kuingilia kati ili kuhakikisha haki inapatikana na kuzuia matukio kama haya yasijirudie.
Hadi sasa, Elizabeth bado anasubiri hatua za kisheria kufanikisha kurejeshewa nyumba yake au kupatiwa malipo stahiki yaliyobaki.
#KonceptTvUpdates