Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameweka wazi msimamo wa chama chake kuhusu kampeni mpya inayoratibiwa na vijana wa CHADEMA (BAVICHA) yenye kauli mbiu “Samia Must Go”. Akizungumza leo kwenye mkutano na wahariri na waandishi wa habari waandamizi uliofanyika katika ofisi ndogo za CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam, Dkt. Nchimbi alikosoa kampeni hiyo akisema haina msingi wowote na ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dkt. Nchimbi alisisitiza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan yupo madarakani kwa mujibu wa Katiba na ataendelea kuhudumu hadi atakapomaliza muda wake wa kikatiba. “Hata wakipiga kelele, ukweli ni kwamba Rais Samia yupo Ikulu kwa mujibu wa Katiba na ataendelea hadi muda wake wa kikatiba utakapomalizika,” alisema Dkt. Nchimbi.
Akifananisha kampeni ya “Samia Must Go” na kampeni zilizowahi kuendeshwa dhidi ya Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Nchimbi alisema kuwa kelele za kumtaka Mbowe aondoke zilishindwa kutokana na kuvunja Katiba ya chama hicho. “Mbowe amebaki kuwa Mwenyekiti kwa kuwa hakuna kampeni iliyoweza kumng’oa kikatiba, na vivyo hivyo, Rais Samia atamaliza muda wake kwa mujibu wa Katiba ya nchi.”
Dkt. Nchimbi alieleza kuwa CCM imejitahidi kuepuka mijadala isiyo na tija na itaendelea kufanya kazi kwa kufuata misingi ya Katiba, huku akiwashauri vijana wa CHADEMA kufuata mfano huo kwa kuheshimu taratibu za kikatiba.
Mkutano huu wa Dkt. Nchimbi umekuja wakati ambapo mijadala ya kisiasa inazidi kushika kasi nchini, huku upinzani ukiendelea kutoa maoni yao kuhusu utawala wa Rais Samia.
#KonceptTvUpdates