Jeshi la Polisi Tanzania limepiga marufuku maandamano yaliyotangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), yaliyopangwa kufanyika tarehe 23 Septemba 2024 katika jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine nchini.
Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa Jeshi la Polisi, David A. Misime, Polisi imeeleza kuwa viongozi wa CHADEMA walitumia mitandao ya kijamii mnamo Septemba 11, 2024, kuwahamasisha wananchi kushiriki maandamano hayo. Polisi imeeleza wasiwasi wake kuhusu nia ya maandamano hayo, hasa katika kipindi hiki ambapo nchi inakabiliwa na changamoto za kitaifa.
Polisi imeeleza kuwa imeanza uchunguzi wa kina juu ya suala hilo na itatoa ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan mara baada ya uchunguzi huo kukamilika. Jeshi hilo limeeleza kuwa kuna jitihada za baadhi ya viongozi wa chama hicho kuhamasisha ghasia, jambo ambalo linaweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi.
“Tunatoa onyo kali kwa viongozi na wafuasi wa CHADEMA kuacha mara moja juhudi za kuhamasisha wananchi kuingia barabarani kwa maandamano yasiyo halali,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo. Polisi wamekumbusha kuwa maandamano hayo yamepigwa marufuku na yeyote atakayeshiriki atakabiliwa na hatua kali za kisheria.
Aidha, Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa wananchi wenye nia ya kulinda amani wasikubali kushawishiwa kujiunga na maandamano hayo haramu na badala yake washirikiane na vyombo vya dola katika kudumisha amani nchini.
#KonceptTvUpdates