Na Mwandishi Wetu
WAKAANGA Samaki wa Soko la Kimataifa la Samaki Feri Jijini Dar es Salaam wamesisitizwa kuweka ulinzi pindi mradi wa ujenzi wa tanki kubwa la kisasa la gesi utakapokamilika ili uweze kuwasaidia kuondokana na changamoto ya gesi ya kupikia.
Akizungumza leo Septemba 14,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa kuutambulisha mradi huo wa ujenzi wa tanki kubwa la kisasa la gesi , Zungu amesema wafanyabiashara hasa wa kukaanga samaki katika soko hilo wamekuwa wakipata hasara ya kununua mitungi ya gesi lakini ni asilimia 45 tu ndio inafanya kazi kutokana na mazingira ya gesi kuganda na kuwa barafu.
“Kutokana na hasara hiyo tumeona uje mradi wa tenki la gesi la jumla ambalo kila mtu atakuwa na luku yake na matumizi yake kwa maana hiyo matumizi ya gesi yatakuwa mazuri lakini kwa gharama nafuu.
“Lakini kikubwa tunaunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kutunza mazingira yetu, moshi wa kuni na moshi wa mkaa unaharibu mazingira yetu katika nchi yetu hivyo tunaungana na Rais pamoja na wadau wetu…
“Tunawashukuru sana kampuni ya Oryx Gas nchini ambayo imekubaliana kwa pamoja kushirikiana na halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kusaidia kundi hili la wafanyabiashara wa kukaanga samaki wapate nishati safi na salama lakini kwa gharama ya fedha wanazotoa.”
Amefafanua mpaka sasa hatua walizochukua kisheria zimekamilika kwa asilimia 90 na hayo yote wanayofanya ni maelekezo ya Rais Dk.Samia kuwatazama wananchi wake kwa jicho la huruma kuhakikisha kila mwananchi anafanya shughuli zake kibiashara kwa gharama ya chini.
“Viongozi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala walifanya jitihada za kuhakikisha mchakato wa ujenzi wa tanki hilo unatekelezwa na walifanya jitihada za kufanikisha kupatikana kwa eneo la mradi huu.Mradi huu umekuja kwa maslahi mapana ya wafanyabiashara , mazingira na taifa kwa ujumla,” amesema Zungu.
Kwa upande Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Ashelly Mbasha amesema mradi huo ni mkubwa ambao unagharimu zaidi ya milioni 300 hadi utakapokamilika na wanategemea kuuanza mapema iwezekanavyo.
“Tunachokiomba Oryx ni ulinzi wa miundombinu mradi utakapoanza kwani tunaweka miundombinu ya gharama kubwa kwa kuwa gesi inataka usalama mkubwa. Kwahiyo tunaomba ulinzi wa hii miundombinu ili iweze kutusaidia wafanyabiashara wote.
“Sisi kama Oryx tutaendelea kushirikiana na Serikali na kipekee nimshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilala kwani huu ni ubunifu mkubwa ambao amekuja nao, kwa kushirikiana na Serikali ya Manispaa ya Ilala ambayo inakwenda kusababisha soko kuwa safi na litakuwa na usalama wa hali ya juuu.
“Kwa hiyo sisi tunaendelea kumpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na kampeni yake hii ya kuhakikisha mpaka mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi.Tunaendelea kuwakaribisha wadau wengine wote kutoka kampuni binafsi,mashirika na taasisi tunafanya kazi pamoja kuhakikisha ajenda ya Rais tunaifikisha pamoja,” amesema Mbasha.
Amesisitiza makubaliano ya awali yameshafikiwa na sasa wako hatua za mwisho na hatimaye kuanza utekelezaji wa mradi hivyo wanashukuru kwa hatua hiyo na kubwa wanaomba ushirikiano wa wafanyabiashara wa soko hilo na wadau ili mradi ukamilike kwa muda uliokusudiwa.
Awali Meya wa Jiji la Dar es Salaam Omary Kumbilamoto amesema Naibu Spika na Mbunge wa Jimbo la Ilala Mussa Zungu anafanya kazi kubwa ya kumsaidia Rais Samia na hayo yanayofanyika katika soko hilo yanatokana na Naibu Spika kupokea maelekezo kutoka kwa Rais ya kuhakikisha wanabadilisha matumizi ya kuni na mkaa na kuingia katika matumizi ya gesi.
“Niwaombe wafanyabiashara tupokee mabadiliko kwani tunajua mabadiliko yanachangamoto lakini natumaini watayalubali muda sio mrefu.Nawashukuru nawashukuru Oryx ambao wanakuja kuleta msaada wa zaidi ya Sh.milioni 300,” amesema Kumbilamoto.
Amempongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelya kwani siku tatu zilizopita ndio tumesaini mkataba wa mradi wa tanki kubwa la gesi ya Oryx huku akisisitiza wanachosubiri ni kuanza utekelezaji kwani vibali vyote vimeshakamilika vya kuruhusu mradi huo.
Aidha amewaomba wafanyabiashara kuwapa ushirikiano Oryx kwani wanachoangalia ni maslahi mapana ya mji wa Dar es Salaam na kuubadilisha lakini wanaenda na kauli ya Rais Dk.Samia ya kuhamasisha nishati safi na hivi sasa dunia inamtambua kama Championi wa mazingira kwahiyo sisi tunawajibu kama wasaidizi wake kumsaidia,
Kumbilamoto amesema mchakato wa kubadilisha mji huo kwa matumizi ya gesi hakuna kipaumbele kingine zaidi ya hicho kwahiyo amesisitiza ushirikiano.