Mhadhiri Mwandamizi kutoka chuo kikuu Kishiriki cha Mkwawa Dkt. Joseph Milinga amesema katika kipindi cha miaka 30 ya Elimu Jumuishi nchini Serikali imeweka kipaumbele katika ujumuishi wa wanafunzi wenye uoni na uandaaji wa walimu katika vyuo vya Ualimu.
Ameyasema hayo wakati akitoa mada kuhusu jinsi watoto wasioona wanavyojumuishwa kwenye kupata huduma ya elimu mchini wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya elimu Jumuishi, yanayofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari maalum Patand , Jijini Arusha
Dkt. Milinga amesema msingi na dhana jumuishi ni mchakato endelevu ambao umetiliwa mkazo kwa muda mrefu hususani kipindi cha Azimio la Salamanka pamoja na kuwepo kwa changamoto kadhaa zinakuwa sehemu ya mchakato wa ujumuishi.
Amefafanua kuwa Tanzania ilisaini mkataba ambao ni Tamko la Salamanka la 1994 na Tamko la Dakar la 2000 inayozitaka kila nchi kutafsiri kwa vitendo na kutekeleza Elimu Jumuishi katika mazingira yake ikiwa ni pamoja na lengo Namba 4 la Malengo Endelevu ya Milenia ya Mwaka 2030 linaloweka msisitizo wa utoaji wa elimu kwa usawa.
Aidha, amesema Tanzania ilianza kutekeleza Elimu jumuishi kupitia Sheria ya Elimu ya 1978 iliyoelekeza upatikanaji wa elimu kwa kila mtoto sambamba na Sera mpya ya Elimu toleo la tatu.
“Tanzania kwa sasa inatekeleza Mkakati wa kitaifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2022 hadi 2026 ambao umelenga kufanikisha utoaji wa Elimu Jumuishi iliyo bora pamoja na ujenzi wa utamaduni jumuishi ndani na nje ya shule. ” amesema Milinga
Dkt. Milinga anasema kundi kubwa la wenye mahitaji maalum ni la uoni pia anasisitiza kwa kusema Serikali peke yake haiwezi kufanikisha azma ya elimu jumuishi na badala yake jitihada za pamoja zinahitajika ili kufikia azimio la Salamanka.