Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mohamed Mchengerwa amesema hakuna mgonjwa anayesafirishwa kwa njia ya pikipiki huku akiwa amewekwa kwenye tenga kupelekwa kupata huduma za Afya.
Mchengerwa ameyasema hayo wakati akitoa salaam za Wizara kwenye mkutano wa hadhara wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wananchi wa Tunduru uliofanyika kwenye wilayani humo Septemba 26 2024.
Mchengerwa akifafanua juu ya taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha mgonjwa akisafirishwa kwenye pikipiki huku akiwa kwenye Tenga na mgonjwa huyo akieleza kuwa hakuna magari ya kusafirishia wagonjwa na kwa yaliyopo huwagharimu wananchi fedha nyingi kwa ajili ya kupata huduma ya magari hayo.
Aidha ameeleza kuwa kwa mwaka jana serikali ilitoa magari ya wagonjwa 535 nchi nzima na yaliyokabidhiwa katika Wilaya hiyo ni magari manne (4) ya kubebea wagonjwa.
Pia amefafanua vituo vilivyopokea magari hayo ni Kituo cha Afya Nakapanya, Matemanga, Mtesi na Kituo cha Afya Nyalasi ambapo magari hayo yanafanya kazi saa 24 na rufaa zote zinaratibiwa kwa utaratibu maalumu na sio kuchangisha wananchi.
“Utaratibu unaotumika kusafirisha wagonjwa nikutumia magari ya kubebea wagonjwa (Ambulaces) na kwa kutumia madereva ngazi ya jamii waliosajiliwa wakati wa mfumo wa M-Mama ambapo mfumo huu unahusika na kusafirisha wakina mama wajawazito na watoto wachanga bila malipo yoyote” ameeleza Mchengerwa.