Baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara Tundu Lissu kudai kuwa kampuni ya Tigo Tanzania ilivujisha taarifa zake za siri na kuwapatia watu waliojaribu kutekeleza jaribio la mauaji dhidi yake mwaka 2017, wamiliki wa kampuni hiyo wamejitokeza na kudai kuwa hawahusiki na madai hayo.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na kampuni ya Honora Tanzania Public Limited ambayo ni wamiliki wa sasa wa kampuni ya mawasiliano ya Tigo imeeleza kuwa kampuni hiyo haihusiki na haitambui chochote kuhusiana na kesi inayoendelea nchini Uingereza ikihusisha kampuni ya Millicom (iliyokuwa inamiliki kampuni ya Tigo Tanzania wakati huo) na aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni hiyo raia wa Uingereza Michael Clifford.
Katika taarifa yake kampuni ya Honora Tanzania Public Limited imeeleza kuwa kampuni ya Millicom ilikuwa inaimiliki kampuni ya mawasiliano ya Tigo Tanzania hadi kufikia mwaka 2022, na kwamba wakati madai yanayotajwa yanatokea mwaka 2017 ni kweli kuwa kampuni hiyo ilikuwa chini yake lakini kwa sasa (wakati huu ambao kesi inaendelea nchini Uingereza) kampuni ya mawasiliano ya Tigo Tanzania haimilikiwi na kampuni ya Millicom kama inavyoelezwa bali inamilikiwa na kampuni ya Honora Tanzania Public Limited, hivyo wamiliki hao wa sasa hawahusiki na madai hayo.
Kampuni ya Honora Tanzania Public Limited inayomiliki kampuni ya mawasiliano ya tiGO Tanzania imeendelea kufafanua kuwa kesi inayoendelea nchini Uingereza haihusishi kampuni ya Tigo Tanzania bali inahusisha kampuni ya Millicom na aliyekuwa mfanyakazi wake.
Aidha, kampuni ya Honora Tanzania Public Limited imeendelea kuwahakikishia wateja wake wote kuwa bado wataendelea kulinda taarifa za wateja wao ingawa imeeleza kuwa haiwezi kuingia ndani kueleza kinachoendelea Mahakamani kuhusu kesi tajwa
“Tunataka kuwahakikishia wateja wetu na wadau wetu kwamba kulinda data zao binafsi kwa kuzingatia sheria na kanuni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bado ni kipaumbele chetu kikuu……Kampuni mama ya sasa ya Tigo Tanzania ambayo ni kampuni ya Honora Tanzania Public Limited haikuwa mmiliki wake wakati tukio lililoripotiwa linatokea” ilisema Honora Tanzania Public Limited Jumatano, Septemba 25.2024.
Akiwa kwenye ofisi za makao makuu ya CHADEMA Mikocheni jijjini Dar es Salaam, Tundu Lissu alidai kuwa kwa kiasi kikubwa kampuni ya Tigo Tanzania ilichangia yeye kushambuliwa kwa risasi kwa kuwa taarifa zake za siri zilitolewa na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo na kuzipeleka kule alikodai kuwa kwa maafisa wa serikali.
Lissu alienda mbali zaidi kwa kueleza kuwa tayari ameshatoa maelekezo kwa Mawakili wake waanze mchakato wa kufungua kesi ya msingi kwa kampuni ya Millicom aliyodai kuwa inamiliki kampuni ya Tigo Tanzania, lakini pia kufungua kesi dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.