Dar es Salaam, Tanzania — Oktoba 31, 2024. Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) imezindua rasmi Ripoti yake ya Uendelevu ya 2024 yenye kaulimbiu ‘Kusimamia Ujumuishwaji na Ushirikishwaji’, mnamo Oktoba 31, 2024. Ripoti hii inaangazia dhamira ya SBL ya kuendeleza mazingira jumuishi ambapo watu wenye asili mbalimbali wanaweza kufanikiwa, kwa kuzingatia kuondoa vikwazo na kuleta athari chanya kwa jamii, wasambazaji, na wadau.
SBL, ikifanya kazi chini ya East African Breweries Limited (EABL), imepanga kutenga rasilimali za kutosha kuwekeza katika jamii kupitia mpango wao wa ‘Spirit of Progress’ – mpango wa ESG unaolenga kuunda jamii endelevu katika maeneo wanayoyahudumia. Tukio hilo liliwakutanisha mamia ya wadau na kufanya mazungumzo kuhusu namna ya kuboresha ushirikiano ili kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa kiuchumi kwa kushughulikia changamoto, fursa, na uboreshaji wa sera.
Shabnam Mallick, Mkuu wa Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), alihudhuria tukio hilo na kutoa mtazamo wake, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano, uboreshaji wa sera, na hatua za pamoja katika kuendeleza usawa wa kijinsia kama nguzo ya uwezeshaji kiuchumi na uendelevu katika taasisi yoyote.
“Ninafurahi kuona hatua kubwa ambazo SBL imepiga katika kukuza usawa wa kijinsia na kuunga mkono wanawake katika nafasi za uongozi. Ninafurahia pia kuona kwamba kampuni imeweka malengo ya matumizi kwa wasambazaji mbalimbali pamoja na ufuatiliaji. Hiki ni kitendo cha makusudi ambacho ni muhimu katika kufikia malengo yetu ya muda mrefu ya uendelevu na kuhakikisha maendeleo yanawafikia wote,” alisema Mallick.
Mwenyekiti wa Bodi ya SBL, Paul Makanza alikazia mbinu zinazotumika kuhakikisha ripoti za uendelevu zinakuwa chachu ya maendeleo kiuchumi Afrika, alisema, ‘Wanawake wanapokuwa na fursa sawa, uchumi unakua, familia zinastawi, na jamii zinaendelea. Tukifunga pengo la kijinsia barani Afrika, inaweza kuongeza dola bilioni 316 kwenye uchumi wetu kufikia mwaka 2025. Huo ndio ukuaji. Na hii ni sehemu ambayo SBL tumedhamiria kuhusika zaidi’.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi, alizungumzia mchango wa kampuni yao kwenye ukuaji jumuishi na uwezeshaji kiuchumi wa makundi maalum nchini, akisema, “Juhudi zetu za ushirikishwaji na usawa zinaakisi dhamira yetu ya kuwezesha makundi yaliyotengwa, ikiwa ni pamoja na wanawake, watoto, na watu wenye ulemavu, ili wafaidike na fursa za kijamii na kiuchumi. Najivunia kuripoti kwamba karibu asilimia 40 ya wakulima tuliowawezesha mwaka huu walikuwa ni wanawake na watu wenye ulemavu ambao wanalima mtama, moja ya viungo muhimu katika uzalishaji wa bia zetu. Kupitia ushirikiano wetu na Sightsavers, tumewaunga mkono zaidi ya wanawake na watu wenye ulemavu 200 katika mkoa wa Singida, tukiwasaidia kukuza mtama kwa ajili ya uzalishaji kwa SBL.”
Ripoti hii inaeleza zaidi mipango ya kimkakati ya SBL inayolenga kuondoa vikwazo vinavyozuia ushirikishwaji na maendeleo, hasa kwa wanawake na watu wenye ulemavu. Mipango hii, ambayo inaambatana na ahadi kubwa za ESG za SBL, inachangia kwa kiasi kikubwa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).
SBL imeendelea kusisitiza nia yake ya kuimarisha juhudi zake za uendelevu ili kuleta athari chanya katika jamii nchini kwa kupitia ushirikiano na washirika, wadau, na jamii kwa ujumla, kuhamasisha mazingira bora ambapo ushirikishi na uwezeshaji kiuchumi ni muhimu katika maendeleo.
MWISHO.