Akiba Commercial Bank imetembelea eneo la ajali ya jengo la biashara lililoporomoka huko Kariakoo, ajali ambayo imesababisha madhara makubwa, ikiwemo majeruhi, uharibifu wa mali, na hata kuangamia. Hayo yalisemwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. Tobha Nguvira, ambaye pia ni msimamizi wa kitengo cha maafa cha mkoa wa Dar es Salaam wakati wa kupokea msaada kutoka Akiba Commercail Bank.
Benki hiyo, imetoa msaada wa katoni za maji kwa ajili ya kusaidia timu ya uokozi inayofanya juhudi kubwa za kuokoa watu waliokumbwa na ajali hiyo mbaya na ya kusikitisha. Ujumbe wa Akiba Commercial Bank uliongozwa na wafanyakazi wa matawi ya Kariakoo pamoja na makao makuu , akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano, Bi. Dora Saria, na Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji, Dkt. Danford Muyango.
Dkt. Muyango aliwahakikishia wateja wa Akiba Commercial Bank ambao huenda wameathirika na janga hilo kwamba benki iko tayari kutoa msaada wa haraka. Aliwataka wateja kufika katika matawi ya benki hiyo mapema ili kutoa taarifa za athari walizopata. Alisisitiza kuwa benki itatoa usaidizi wa tathmini ya kina kuhusu huduma za bima na kuanzisha utaratibu wa marejesho ya mikopo yao kulingana na hali ya mpito baada ya janga.
Tukio hili linaonyesha jinsi Akiba Commercial Bank inavyojitoa si tu kuhudumia wateja wake bali pia kushiriki katika juhudi za kijamii wakati wa dharura na majanga, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kujenga jamii imara na yenye mshikamano.