Mataifa matatu ya Afrika Magharibi yakiongozwa kijeshi yametangaza kujiondoa mara moja katika muungano wa kikanda wa ECOWAS, yakituhumu baraza hilo kuwa tishio kwa wanachama wake.
Niger, Mali na Burkina Faso “zinaamua kwa uhuru kamili juu ya kujiondoa mara moja” kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), ilieleza taarifa ya pamoja iliyochapishwa Jumapili.
ECOWAS “chini ya ushawishi wa mataifa ya kigeni, kwa kusaliti kanuni zake zilizoanzishwa, imekuwa tishio kwa nchi wanachama na wakazi wake”, ilieleza taarifa hiyo.
Nchi hizo tatu zilishutumu chombo cha kikanda kwa kushindwa kuunga mkono mapambano yao dhidi ya “ugaidi na ukosefu wa usalama”, huku zikiwekewa “vikwazo haramu, vya kinyama na kutowajibika”.
ECOWAS ilisema katika taarifa kwamba haijaarifiwa kuhusu uamuzi wa nchi hizo kujiondoa kwenye umoja huo. Itifaki yake inasema kwamba uondoaji huchukua hadi mwaka mmoja kukamilika.
#KonceptTvUpdates