Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekuwa kitovu cha umahiri katika tathmini na usajili wa dawa barani Afrika na kuwa na maabara inayotumika kutoa mafunzo kwa mamlaka za udhibiti barani Afrika.
Hayo yamesemwa leo Februari 12, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus Nyongo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Shughuli za Kamati kwa mwaka 2023 katika bunge la 12, mkutano wa 14 kikao cha 10 bungeni jijini Dodoma Mhe.
Nyongo amesema Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imepata cheti cha umahiri cha kiwango cha ISO 9001: 2015 katika mifumo ya utendaji ya udhibiti wa bidhaa na kuendelea kushikilia cheti hicho Mwaka hadi Mwaka.
Amesema TMDA imepanua wigo wa huduma za maabara kwa kujenga maabara ya kisasa ya uchunguzi wa dawa na vitendanishi Kanda ya Ziwa, Mwanza na uchunguzi wa dawa za mitishamba na bidhaa za tumbaku Kanda ya kati Dodoma huku akishauri uwepo wa mfumo mahiri wa TEHAMA wa kupokea na kuchakata maombi ya usajili wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi (Regulatory Information Management System -RIMS)