Zaidi ya shilingi Bilioni 15 zimetolewa na Serikali kuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera na kuchangia ukuaji wa sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Wakili Stephen Byabato wakati akiwautubia wananchi wa manispaa ya Bukoba kwenye Mkutano wa hadhara umefanyika katika viwanja vya Soko kuu la Manispaa hiyo tarehe 14 April, 2024.
Wakili Byabato amesema kuwa katika miaka 3 ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo inahitimishwa mwezi huu serikali ya awamu ya 6 imetoa fedha nyingi ambazo zilisaidia kuboresha mindomibinu ya elimu, Barabara, huduma za afya na Uchumi kwa wakazi wa Jimbo la Bukoba mjini, Amesema kuwa kupitia fedha hizo baadhi ya maeneo ambayo hayakuwa na shule yamepata huduma hiyo kwa kujengewa shule mpya za msingi na sekondari sambamba na kuanzisha huduma za Viwanda, Biashara na uwekezaji.
Miradi mingine ya mafanikio ni pamoja na uwekaji wa Taa za Barabarani, Marekebisho katika Soko kuu, Usafishaji wa mto Kanoni, Ujenzi wa Hospitali ya wilaya iliyopo Nshambya pamoja na uunganishaji umeme kwa wananchi kupitia miradi inayotekelezwa na wakala wa umeme vijijini – REA.
Kufuatia kuwepo kwa mafanikio hayo sambamba na uwepo wa mahitaji mengine ya maendeleo, Wakili Byabato ametumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa .
Wakati huo huo Wakili Byabato amezindua ligi ya Mpira ambapo ametoa mipira minne kwa kila kata pamoja na kiasi cha shilingi laki mbili ambazo zimekabidhiwa kwa Madiwani wa kata zote 14 za Jimbo hilo kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ligi hiyo Pia amekabidhi rasmi kwa wananchi gari la wagonjwa ambalo lilitolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan .