Balozi wa Ethiopia nchini Somalia, Mukhtar Mohamed Ware, amearifiwa kuondoka nchini humo ndani ya saa 72 zijazo.
Vile vile, balozi za Ethiopia katika maeneo ya Hargeisa na Garowe zinahitajika kufungwa ndani ya siku 7.
Aidha, Somalia imefunga balozi zake ndogo katika maeneo ya Puntland na Somaliland siku ya Alhamisi.
Katika taarifa yake, Somalia imeishutumu serikali ya Ethiopia kwa kuingilia masuala ya ndani ya Somalia.
Hisi Ganni, waziri wa serikali ofisi ya waziri mkuu alisema:
‘’Kuanzia leo, tarehe 04 Aprili 2024, Serikali ya Somalia imefunga na kubatilisha kibali cha kuendesha balozi ndogo za Serikali ya Ethiopia katika miji ya Garowe na Hargeisa, na lazima ifungwe ndani ya wiki moja. Wanadiplomasia na wafanyakazi wa serikali ya Ethiopia wanaofanya kazi katika balozi mbili katika miji iliyotajwa lazima waondoke nchini humo ndani ya wiki moja”.
Haya yamejiri siku moja tu baada ya jimbo linalojitawala la Puntland kutangaza makubaliano mapya ya ushirikiano na Ethiopia.
Maafisa kutoka Somalia walithibitisha hatua hizi zimechukuliwa kujibu kuhusika kwa Ethiopia katika makubaliano hayo yenye kuhusisha eneo linalozozaniwa la Somaliland.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud ameshutumu makubaliano hayo kuwa ni kinyume cha sheria, akionya kuhusu hatua za kujihami iwapo Ethiopia itaendelea.
Kufungwa kwa ubalozi wa Ethiopia kunaonyesha mpasuko mkubwa uliopo kati ya nchi hizo mbili, na athari zinazowezekana kutokea kwa wanajeshi wa Ethiopia waliopo Somalia chini ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika.
Chanzo; BBC Swahili
#KonceptTvUpdates