Kigoma – April 17, 2024, Serikali ya Marekani imezindua mradi wa USAID Lishe wenye thamani ya dola milioni 40, unaoendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya Marekani, serikali ya Tanzania na sekta binafsi katika kupanua upatikanaji wa vyakula vyenye lishe na huduma za maji safi kwa jamii.
Hivi sasa, asilimia 30 ya wanawake na watoto nchini Tanzania wanakabiliwa na viwango vya juu vya utapiamlo. Jamii zinapambana kupata vyakula bora na uchache wa msimu wa kilimo pamoja na wazazi kukosa uelewa wa mpangilio wa lishe bora kwa watoto na upatikanaji wa huduma za lishe katika vituo vya afya ya jamii. Maeneo ya vijijini yanakabiliwa na upungufu wa maji safi na huduma za vyoo, jambo linalochangia kuendelea kwa ugonjwa wa utapiamlo.
Mradi wa USAID Lishe utafanya kazi kwa kushirikiana na washirika wa Serikali ya Tanzania pamoja na sekta binafsi kutatua changamoto hizo.
“Kupitia Mradi wa USAID Lishe, tunaziwezesha jamii kufanya mabadiliko yanayoonekana katika afya na ustawi wao,” alisema Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la USAID nchini Tanzania Bw. Craig Hart. “Kwa pamoja, tunaongeza uelewa kuhusu lishe na usafi wa mazingira: tunawekeza katika miradi inayoleta mabadiliko ya kweli na ya kudumu.”
Pamoja na mradi huu, uwekezaji wa USAID katika kuboresha lishe nchini Tanzania umefikia dola milioni 100 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Miaka 15 iliyopita, serikali ya Marekani kupitia USAID, iliwekeza dola bilioni 3.2 katika afya ya Watanzania, ikiwa ni pamoja na afya ya mama na mtoto, kupambana na VVU/UKIMWI, kinga na matibabu ya kifua kikuu, uzazi wa mpango, malaria na zaidi.
Mradi wa USAID Lishe pia utaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi hasa vijijini; kuboresha utaratibu wa kutoa maji taka katika mashimo maeneo ya mijini; na kuendeleza huduma za usafi wa mazingira zinazopatikana nchini na upatikanaji wa bidhaa za usafi kama vile vyoo salama vilivyoundwa kupunguza uwezo wa wadudu kueneza magonjwa.
Kwa ujumla, katika miaka mitano ijayo, mradi wa USAID Lishe utaongeza upatikanaji wa chakula bora, kuelimisha jamii juu ya lishe bora, kuzuia magonjwa yatokanayo na maji machafu, na kusaidia wahudumu wa afya 3,000 katika kliniki 1,300 kupunguza utapiamlo. Mradi huo utaboresha afya na maisha ya watoto na wanawake zaidi ya milioni mbili kutoka wilaya 29 za mikoa ya Kigoma, Katavi, Njombe, Rukwa na Songwe nchini Tanzania.