NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata kilogramu 767.2 za dawa za kulevya katika operesheni zilizofanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga kuanzia Aprili 4 hadi 18,2024.
Kati ya dawa hizo zilizokamatwa, heroin ni kilogramu 233.2, methamphetamine kilogramu 525.67 na skanka kilogramu 8.33.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 22,2024 Jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo amesema watuhumiwa 21 wamekamatwa kuhusika na dawa hizo za kulevya, baadhi yao wamefikishwa mahakamani na wengine watafikishwa taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Aidha amesema Aprili 4, 2024 katika eneo la Mikwajuni Jijini Tanga watuhumiwa wawili walikamatwa wakiwa na dawa za kukevya aina ya heroin kiasi cha gramu 329.412.
Amesema operesheni iliyofanyika Aprili 10 katika eneo la Zinga Bagamoyo mkoani Pwani, zilikamatwa kilogramu 424.84 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine.
“Watuhumiwa watatu walikamatwa kuhusika na dawa hizi aina ya methamphetamine na katika tarehe hiyohiyo katika eneo la Kunduchi Jijini Dar es Salaam, alikamatwa mtuhumiwa mmoja akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha gramu 158.24”. Amesema
Ameeleza kuwa Aprili 8,2024 katika eneo la Wailes Temeke Jijini Dar es Salaam, zilikamatwa kilogramu 1.49 za dawa za kulevya aina ya skanka ambapo watuhumiwa wawili walikamatwa kuhusika na dawa hizo.
Pia ameeleza kuwa Aprili 16,2024 katika kata ya Kunduchi Jijin Dar es Salaam zilikamatwa kilogramu 232.69 za dawa za kulevya aina ya heroin na kilogramu 100.83 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine zilizokuwa zinaingizwa nchini kupitia Bahari ya Hindi ambapo watuhumiwa tisa waliokamatwa katika eneo hilo.
Amesema baadhi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya wameendelea kutumia vifungashio vyenye majina ya aina mbalimbali ya kahawa na chai kama vile organic coffee, cocoa, na green tea kwa lengo la kukwepa kutiliwa mashaka wakati wa kusafirisha dawa za kulevya.