Kilimanjaro, 24 Aprili 2024. Benki ya Exim imekabidhii seti ya vitanda kwa Shule ya Jeshi la Polisi Tanzania iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro kama sehemu ya mchango wa Exim Bank katika jamii ikiwemo ulinzi na usalama wa Watanzania na mali zao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko, Stanley Kafu alisema, “Kupitia mkakati wetu wa kurudisha kwa jamii unayojulikana kama Exim Cares na kama ishara ya mashirikiano yetu ya muda mrefu, tunayo furaha kuchangia vitanda 40 kwa Shule ya Jeshi la Polisi Tanzania ya hapa Moshi.”
Exim bank inaamini mchango huu utasaidia kuboresha mazingira ya mafunzo kwa maafisa wa polisi ili wapate mafunzo bora yatakayochangia kuboresha jeshi la polisi katika majukumu yake ya kuwahakikishia ulinzi na usalama Watanzania wote na mali zao.
“Ushirikiano wetu na Jeshi la Polisi haujaanza leo, mwaka jana Exim Bank tumeingia makubaliano na Jeshi la Polisi Tanzania yenye lengo la kuwezesha utoaji wa mikopo ya masharti nafuu kwa askari polisi kupitia programu yetu maalumu ijulikanayo kama ‘Wafanyakazi Loan’”, aliongeza Kafu.
Akifafanua zaidi Kafu alisema kuwa kupitia ‘Wafanyakazi Loan’, askari polisi wanaweza kukopa kuanzia shilingi milioni moja hadi shilingi milioni 160 ambayo inaweza kurejeshwa kati ya miezi 6 hadi miezi 96 kutegemeana na ahadi ya mkopaji ambayo inaweza kutumika kutekeleza ndoto za mkopaji ikiwa ni pamoja kupata mkopo wa nyumba, kununua magari na kulipia ada ya masomo ili kujiendeleza kielimu.
Exim Bank imedhamiria kuendelea kushirikiana na serikali na vyombo vyake vya usalama kuhakikisha ustawi unakuwepo katika sekta mbalimbali ikiwemo usalama, afya, uchumi, na kuboresha maisha ya Watanzania wote bila ubaguzi wa namna yoyote.
-MWISHO-