Baadhi ya wachezaji wa timu ya Yanga wakiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana wakitokea katika ziara ya michezo ya kirafiki nchini Rwanda
—
MASHABIKI wa soka nchini wameendelea kutoamini macho yao, baada ya Mabingwa wa Soka Afrika Mashariki na Kati Yanga jana kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere jijini Dar es Salaam ikitokea Kigali, Rwanda, bila ya beki wake mpya aliyecheza mechi za kirafiki nchini humo Mbuyu Twite.
Twite aliyesajiliwa na Yanga akiwa Rwanda na kisha kubaki huko hadi alipoungana na timu nchini humo na kucheza mechi hizo za kirafiki, alitarajiwa kutua jijini na Wanajangwani hao, ambapo mashabiki wa Yanga na wa Simba walisubiri ujio wake.
Kusubiriwa kwa hamu kwa Twite kunatokana na mkanganyiko aliozua katika usajili wake, ambapo awali alisajiliwa na kutambulishwa na Simba akitokea APR ya Rwanda alikokuwa akicheza kwa mkopo, kabla ya Yanga kutibua dili hilo na kumsainisha kupitia klabu yake ya zamani ya Lupopo ya DRC.
Licha ya kutowasilisha jina lake kwa TFF, Simba imeendelea kulia na Twite iliyemtangaza kuwa tapeli na kumfungulia jalada (RB) la wizi wa kuaminika wa dola za Kimarekani 30,000 za usajili, huku ikimtaka kurejesha fedha hizo mwenyewe kama alivyopewa.
Akizungumza na waandishi wa habari uwanjani hapo wakati msafara wa watu zaidi ya 40 Yanga, wakiwamo wachezaji 28 ulipopokelewa, Katibu Mkuu wa Yanga Mwesigwa Celestine, alisema kuwa, Twite atawasili nchini wakati wowote na kuwa amebaki Kigali akikamilisha baadhi ya mambo.
“Hakuna cha kumtish Twite kiasi cha kutoungana nasi kuja Dar, kuna taratibu muhimu anashugulikia. Atatua nchi wakati wowote na tutakuwa naye katika pambano letu na Coastal Union hapo Jumamosi,” alisema Mwesigwa akikana habari zilizozagaa uwanjani hapo kuwa alihofia kutiwa mikononi na Simba.
chanzo::hakingowi