TABIA ya staa wa filamu za Kibongo, Jacqueline
Wolper kubadilibadili dini mara kwa mara imeonekana kuwakera watu
mbalimbali akiwemo Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum
ambaye amemcharukia vikali.
Wolper kiimani ni Mkristo lakini hivi karibuni alibadili na kuwa
Muislam kabla ya kurejea tena kwenye imani yake ya awali ya ukristo.
Sababu ya Wolper kubadili dini ilikuwa ni kufunga ndoa na aliyekuwa
mchumba wake Abdallah Mtoro ‘Dalas’, walipoachana akaamua kurudi kwenye
ukristo.
Akizungumza na Risasi Jumamosi juzikati, Shehe Salum, alisema Wolper
anapaswa kujichunguza na kubadilika haraka kwani kitendo anachofanya ni
kinyume na taratibu za dini.
“Siyo vizuri hata kidogo na hata dini zote zinakemea kitendo cha kuchezeachezea dini kwani ni chukizo kwa Mungu.
“Kwa upande wa Dini ya Kiislamu,
kuna sheria kali zaidi kwa mtu akionekana na tabia hiyo, anaweza hata
kuuawa hivyo wanaofanya mchezo huo waache kwani siyo vizuri. Huko ni
kumfanyia Mungu dhihaka,” alisema Shehe Salum na kuongeza:
“Unajua suala la imani ni kitu
kinachomhusu mtu binafsi, ni vyema kufanya uamuzi wa hakika na kushika
njia moja na siyo kufanya dhihaka na dini ya Mwenyezi Mungu. Ni kitu
kibaya sana.”
Naye Juma Suleiman, mkazi wa Ilala, jijini Dar es Salaam alimwambia
mwandishi wetu kuwa, katika imani ya kiislam kunakatazwa watu kucheza na
dini huku akisisitiza anayefanya hivyo anaweza kulaaniwa.
“Dini siyo kitu cha kuchezea, ni daraja la kumfikisha mtu
kwenye haki, si mahala pa kuingia na kutoka, kuingia na kutoka. Huko ni
kucheza na Mungu. Namshauri huyo mtoto (akimaanisha Wolper) abadilike.
Asifanye mchezo na imani, Mungu anaweza kumlaani kwa kumchezea,” alisema Suleiman.