MTANGAZAJI maarufu wa redio, Gardner G. Habash kwa mara ya kwanza amefichua ukweli wa makubaliano waliyofikia na mwanamuziki maarufu nchini, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ ya kutozungumza na vyombo vya habari kuhusu taarifa zinazodai kuvunjika au kutengana kwao kindoa.
Wakati Gardner akisita kueleza bayana kuhusu taarifa za kutengana kwake na Jide, taarifa ambazo gazeti hili limezithibitisha zinaeleza kwamba tayari mwanamuziki huyo ameshamuondoa ‘mumewe’ huyo katika nafasi ya umeneja ambayo amekuwa akiishikilia kwa miaka mingi sasa.
Meneja mpya wa Jaydee ambaye amerithi mikoba ya Gardner ni mwanamuziki wa miondoko ya ragga, Webiro Noel Wassira anayejulikana kisanii kwa jina la ‘Wakazi’.
Wakazi ambaye alilithibitishia gazeti hili kwamba yeye ndiye meneja mpya wa Jide, anao uhusiano wa kindugu na mwanamuziki huyo ambaye nyota yake imekuwa iking’ara kwa miaka mingi sasa ndani na nje ya Tanzania.
Kwa upande wake, Gardner alipotakiwa kueleza kuhusu taarifa hizi, hakuwa tayari kuthibitisha zaidi ya kusema kwamba, Jide na yeye wote hawakuwa tayari kulizungumzia hili.
“Ulitaka kujua kuhusiana na Jaydee au ulitaka kujua kuhusiana na mimi?Kama suala ni hilo, Lady Jaydee hayuko tayari kuzungumzia hilo kwa kuwa tumekubaliana kutolizungumzia hilo,” alieleza Gardner.
Katika mahojiano hayo, Gardner ambaye ameishi na Jaydee katika ndoa waliyofunga kiserikali miaka tisa iliyopita, alishikilia msimamo wa kutotaka kueleza lolote kwa undani kuhusu undani wa mahusiano yake na Jide.
Mazungumzo kati ya Mwandishi wetu na Gardner yalikuwa kama ifuatavyo;
MTANZANIA Jumamosi: Kaka salama?, hapa ni chumba cha habari cha Magazeti ya New Habari (2006) Ltd. Kwa muda mrefu kumekuwa na tetesi za wewe kuachana na mkeo Jaydee na sasa jambo hili limethibitishwa na mmoja wa wanafamilia yenu, pengine hili sasa unalizungumziaje vipi Jaydee uko naye karibu?.
Gardner: Kwa sasa sipo karibu na Jaydee, nipo mbali naye maana nipo kazini, pili Jaydee mwenyewe hataki jambo hili nilizungumzie kwenye vyombo vya hbari na wala hayuko tayari kulizungumza.
MTANZANIA Jumamosi: Lakini wewe si ndiye meneja wake?
MTANZANIA Jumamosi: Ulitaka kujua kuhusiana na Jaydee au ulitaka kujua kuhusiana na mimi juu ya Jaydee, kama suala la Lady Jaydee hayuko tayari kuzungumzia hilo kwa kuwa tumekubaliana kutolizungumzia hilo mimi wala yeye na sasa nipo kazini, basi.
Wakati Gardner akitoa kauli hizo tata, taarifa kutoka kwa watu walio karibu na wanandoa hao zinaeleza kuwa, kutengana kwa wawili hao kunatokana na kutofautiana kwao katika matumizi ya fedha, ulevi, na mmoja wao kutokuwa muaminifu wakati wakiwa ndani ya ndoa.
Taarifa hizo zinaeleza kwamba, licha ya wawili hao kutengana, bado hawajapeana talaka kwa sababu suala hilo ni la kisheria na wao bado hawajaamua kufika kwenye vyombo vya kisheria.
“Wametengana na Lady Jaydee anajiandaa kuhamia katika nyumba yake nyingine ambayo aliionyesha katika kipindi chake cha ‘Diary ya Lady Jaydee’ akiwa anaifanyia usafi wakati Gardner naye anadaiwa kupanga maeneo ya Mwananyamala baada ya kuishi kwa ndugu zake kwa muda,” kilisema chanzo hicho.
Wakati Wakazi akikiri kwamba yeye ndiye meneja mpya wa Jaydee hakuwa tayari kueleza lolote kuhusu ndoa ya nduguye na Gardner kwa maelezo kwamba yeye si msemaji wao katika masuala ya mapenzi na ndoa yao.
“Mimi sijui chochote, maana nilipokwenda Marekani niliwaacha wakiwa wachumba, lakini nilipokuwa huko nikasikia wameoana, niliporudi nikawakuta tayari wapo katika ndoa na nimeanza kazi ya umeneja wa Jaydee si muda mrefu, hivyo sijui mahusiano yao ya ndani labda muwaulize wenyewe,’’ alijibu Wakazi, lakini alipoombwa namba ya simu ya Jaydee anayoitumia sasa baada ya zile tulizonazo kutopatikana aligoma kuitoa.
Hata hivyo, chanzo kingine kilidai kuwa, yeye kama mwanafamilia ya Lady Jaydee na Gardner ameheshimu makubaliano ya kutengana kwao.
Chanzo hicho kilidai kuwa hatua ya Gardner kuonekana kupitia kipindi cha Mikasi kinachorushwa na Kituo cha Chanel 5, ilitokana na kitendo cha Jaydee kukataa kwenda kwenye kipindi hicho akihofia kuulizwa swali hilo kuhusu ndoa yao.
“Baada ya waandaji wa kipindi cha Mikasi kumkosa Jaydee wakaamua kumualika Gardner” kilisema chanzo chetu hicho.
Katika kipindi hicho cha Mikasi, Gardner alionyesha wazi kuwa na mgogoro na mke wake huyo, kwani kila alipoulizwa na mtangazaji wa kipindi hicho Salama Jabir kuhusiana na jambo lolote linalomuhusu Jaydee alikataa kulizungumzia huku akitaa kumuita mkewe, akitaka aitwe Jaydee.
Taarifa zinadai kuwa kuwa baada ya Jaydee kumtosa Gardner ameamua kumuweka ndugu yake huyo kuwa Meneja wake kwa kuwa yupo vizuri katika kujieleza.
“Lakini pia ni mtu anayemfahamu muziki kwa mapana yake na pia ni mtu wa tungi (pombe) kama alivyokuwa meneja wake aliyeachana naye,” kilieleza chanzo hicho.
Chanzo hicho kilidai kuwa zamani Jaydee akigombana na mumewe alikuwa akitumia muda mwingi kulia na kumtungia nyimbo lakini kwa sasa ameamua kusimama peke yake na kufanya shughuli zake bila kukubali maumivu.
“Kwa sasa Jaydee si yule wa zamani aliyekuwa akilialia kila alipoumizwa, siku hizi Jaydee anajua kuvumilia na kusahau maumivu, kisha anaachana nayo na kufanya mambo mengine, Jaydee ni mpya siku hizi haliilii hovyo,’’ kilieleza chanzo chetu hicho.
CHANZO, MTANZANIA