Dar es Salaam Juni 28, 2016–Tigo Tanzania imetangaza kwamba wateja kutoka mitandao yote hivi sasa wanaweza kutuma na kupokea pesa kwa mteja yeyote wa Tigo nchini kupitia huduma salama na ya uhakika ya Tigo Pesa.
Hatua hiyo imetangazwa wakati wa kuzindua kampeni mpya inayojulikana, ‘NITIGOPESA’ ambayo lengo lake kuu ni kuhakikisha wateja kutoka mitandao yote mikubwa ya simu wanaweza kufanya huduma zao za fedha kwa njia ya simu pamoja na wateja wa Tigo Pesa na wafanya biashara nchini Tanzania.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa Huduma za Fedha, Ruan Swanepoel alisema kuwa Tigo imejikita kuanzisha jamii isiyo na tozo ambapo mteja yeyote anaweza kufurahia malipo mbadala na kufurahia huduma wanazozimudu na za uhakika. Ubunifu huu uliojikita kwa mteja unaangalia ujumuishi wa kifedha kwani unasaidia kutoa pesa zaidi katika mfumo wa kawaida wa kifedha na kuchangia katika kuboresha maisha ya wateja kwa kurahisisha shughuli zinazohitaji pesa.
Alisema kwamba Tigo imewekeza zaidi ya dola milioni 15 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita katika kuboresha jukwaa na huduma zake kufikia ngazi ya kimataifa ili kuendelea kutoa huduma zinazofikiwa, za uhakika, salama na sahihi ambapo wateja kutoka mitandao yote mikubwa ya simu wataweza kupata muda sahihi na mwitiko usio na kasoro kutoka huduma ya Tigo Pesa, na hivyo kufanya shughuli zao za kifedha kufanyika kwa urahisi na kwa kasi.
“Kuanzia sasa na kuendelea mitandao mingine ya fedha kwa njia ya simu kama vile M-Pesa, Airtel Money na EasyPesa itaweza kufanya shughuli zake na Tigo Pesa kupitia ununuzi na ulipaji kutoka mtandao wetu mpana wa wafanyabiashara wa Tigo Pesa ambao umeenea kote nchini,” alisema Swanepoel.
Inaweza kurejewa kwamba mwanzoni mwa mwaka huu huduma ya Tigo Pesa ilikamilisha uendeshaji wa pamoja na waendeshaji wengine wa huduma za kifedha pamoja na mabenki nchini Tanzania katika kuzifanya huduma zake kufikiwa na watu wengi zaidi.