Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imepiga kalenda kusikiliza maombi ya kuchunguza utata wa umri halisi wa msanii wa filamu nchini Elizabeth Michael (18) ‘Lulu’ huku mshtakiwa akidai kuwa na umri wa miaka (17) tofauti na hati ya mashtaka dhidi ya tuhuma zinazomkabili za mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba (28) hadi Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi wa mapitio ya maombi hayo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 17, mwaka huu itakapotajwa mahakamani hapo.
Katika hatua nyingine mawakili wa pande zote mbili wanasubiri wito kutoka Mahakama ya Rufani kwa ajili ya kusikiliza mapitio ya maombi ya utata wa umri wa msanii huyo pamoja na jalada lake kupangiwa jaji wa kusikiliza mapitio hayo.
Awali upande wa Jamhuri uliwasilisha maombi Mahakama ya Rufani wakitaka ifanye mapitio ya uamuzi uliotolewa na wa Jaji Dkt. Fauz Twaib kukubali kusikiliza maombi hayo katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Keneddy Fungamtama, Fullujens Massawe na Peter Kibatala, waliwasilisha hati ya dharura wakiomba mahakama hiyo kusikiliza maombi hayo haraka na kuyatolea uamuzi.
Mapema mahakama kuu pande zote mbili ziliamriwa kuwasilisha vielelezo dhidi maombi hayo ambapo baada ya hatua hiyo, upande wa Jamhuri ulipeleka maombi Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Jaji Dkt. Twaib kusikiliza maombi hayo.
Katika maombi hayo, Mshtakiwa anadai kuwa umri wake ni miaka (17) na sio miaka (18) kama ilivyoandikwa kwenye hati ya mashtaka ambapo ameomba mahakama kuu kuchunguza utata huo na kuyatolewa maamuzi maombi yake.
Upande wa Jamhuri unawakilishwa na Mawakili wa Serikali Shadrack Kimaro akisaidiana na Elizabeth Kaganda huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Mawakili wa utetezi Massawe, Kibatala na Fungamtama.
Katika kesi ya msingi, Lulu anadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka huu Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, alimuua Kanumba.
Source: NIPASHE