ALIYEKUWA
Kocha Mkuu wa timu ya Azam FC, Stewart Hall amepata ulaji mpya baada ya
jana kujiunga na Klabu ya Sunderland AFC ya Uingereza akiwa Meneja wa
‘Kidongo Chekundu Sports Park’ pamoja na Kituo cha Michezo cha Elite
Sports Academy vinavyojengwa Dar es Salaam.
Vituo vyote hivyo
viwili vitakuwa chini ya Kampuni ya kufua umeme ya Symbion Power
inayoshirikiana na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England, katika masuala
mbalimbali ya ukuzaji wa vipaji vya michezo ambapo moja ya mikakati yake
ni kujenga vituo mbalimbali vya michezo nchini kikiwamo cha Kidongo
Chekundu.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Dar es
Salaam na Kitengo cha Mahusiano ya Umma cha Symbion Power, ikimnukuu
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Symbion Tanzania, Peter Gathercole, ilisema Hall
ambaye ni Mwingereza amesaini mkataba na kampuni hiyo bila kueleza ni wa
muda gani.
“Stewart Hall, kocha wa soka Mwingereza, atajiunga na
Symbion Power, kampuni kubwa ya kuzalisha umeme nchini, Sunderland AFC
kutoka Uingereza, na Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo,
kama Meneja wa Kidongo Chekundu Sports Park pamoja na Elite Football
Academy katika Jiji la Dar es Salaam,” ilisema taarifa ya Ofisa Mtendaji
Mkuu huyo wa Sympion Power Tanzania.
Aidha, ilimnukuu Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Sunderland AFC, Margaret Byrne akisema: “Tumefurahishwa
kuona mradi wa kituo cha michezo unaokwenda kwa kasi. Uteuzi wa Stewart
ni maendeleo ya kusisimua na tunajiandaa kuona juhudi kubwa kwa kila
moja anayehusika ili kuleta matunda katika siku za usoni.”
Akizungumza
jana Dar es Salaam, Hall alisema: “Mradi huu utaboresha haraka ubora wa
wachezaji chipukizi katika ngazi ya klabu na timu za Taifa. Chipukizi
watafundishwa masuala ya kiufundi, mbinu, kimwili na mahitaji ya kiakili
katika soka ya kisasa. “Kutakuwa na programu iliyo sheheni ya ukocha.
Nimefurahishwa kuhusu fursa ambazo zitaletwa kwa ajili ya Watanzania.
Wachezaji bora watapewa fursa ya kunolewa katika Kituo cha Michezo cha
Sunderland Academy of Light nchini Uingereza.”
Hall mwenye leseni
ya ukocha ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) na kuwa Mkufunzi wa
shirikisho hilo, alikuwa Kocha Mkuu wa Azam FC hadi kumalizika kwa
mzunguko wa Ligi Kuu ya Bara, Novemba 7, mwaka huu walipoachana na klabu
hiyo kwa makubaliano ya pamoja.
Amewahi kuifundisha timu ya soka
ya Taifa ya Zanzibar, na pia ni aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha
Soka cha timu ya Birmingham City ya Uingereza.
Pia amewahi
kufundisha soka akiwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Saint Vincent na
Grenadines pamoja na Pune FC ya India na Sofapaka ya Kenya.
Baada
ya kuachana na Azam FC, minong’ono ilienea katika duru za soka nchini
kwamba anakwenda katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa
Mkurugenzi wa Ufundi, jambo linalothibitika kuwa si kweli.
Kwa
upande wake, Ofisa Mtendaji wa Sympion Power Tanzania, Gathercole
alisema mradi wa Kidongo Chekundu Sports Park, utakuwa wazi kwa watu
wote ambao watakuwa wanacheza soka katika uwanja wenye nyasi bandia
usiku pamoja na viwanja vidogo vitano, vya umri maalumu.
Kituo
hicho kitakuwa na vyumba vya kubadilishia nguo, chumba cha madaktari
chenye vifaa vya kisasa na mgahawa. Gathercole alisema ujenzi wake
utaanza mwezi huu.
Hivi karibuni, Serikali kupitia kwa Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara ilitangaza
kujengwa kwa kituo hicho, hatua iliyotokana na matunda ya ziara ya Rais
Jakaya Kikwete na ujumbe wake katika kituo cha soka cha Sunderland,
England, Juni mwaka huu.