Kiu ya mashabiki wa Man U huenda ikaisha wiki ijayo
Mashabiki wa Man U wamekuwa wakisubiri kwa hamu kubwa kutangazwa kwa mrithi wa kocha aliyetimuliwa katika klabu hiyo David Moyes. Kocha wa timu ya taifa ya Uholanzi Louis Van Gaal ndiye hasa anayesubiriwa baada ya kufanya mazungumzo na Mashetani hao wekundu. Kumekuwa na zuga zuga za hapa na pale katika hatua za kumtangaza rasmi kocha huyo Mholanzi mwenye umri wa miaka 62, na ambaye mbali na kuzichezea timu mbalimbali kama Royal Antwerp, Telstar, Sparta Rotterdam na AZ tangu akiwa na umri wa miaka 19 pia ni mwalimu wa mpira ambaye amezifundisha timu mbalimbali kwa mafanikio.
Van Gaal alianza kazi ya ukocha mwaka 1986 akiwa kocha msaidizi katika klabu ya AZ mpaka 1988, aliteuliwa kuwa kocha msaidizi wa Ajax kuanzia mwaka 1988-1991, na hatimaye kocha mkuu katika timu hiyo ya Ajax kuanzia 1991-1997. Barcelona ilimpa kibarua Van Gaal kuanzia 1997-2000, Uholanzi walimpa kibarua cha kuinoa timu yake hiyo ya taifa 2000-2002 ingawa alishindwa kufuzu kwa kombe la Dunia. Barcelona waliihitaji huduma ya Van Gaal tena kwani 2002 walimrudisha na kumtumia kwa msimu mmoja tu. 2005-2009 AZ walimpa kibarua Van Gaal kama manager mkuu na baadaye kuhamia Bayern Munich 2009-2011. Timu ya taifa ya Uholanzi walifurahishwa na uwezo wake tena na kumtangaza kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa kwa mara ya pili kuanzia 2012- hadi sasa.
Katika vikosi vyote alivyovinaoa alichukua vikombe vya ligi kuu na kikombe cha Ulaya pamoja na Ligi ya Mabingwa akiwa na Ajax. Bodi ya utawala ya Man U inatarajiwa kumtangaza Van Gaal kama mrithi wa DAvid Moyes wiki ijayo.