Lionel Messi ameingoza Argentina kuiadabisha timu ya taifa ya Trindad & Tobago. Katika mchezo huo uliopigwa huko Argentina, ulimalizika kwa wenyeji Argentina kupata ushindi wa 3-0.
Argentina wakiwa chini ya kocha mkuu Alejandro Sabella wameweka matumaini ya kufanya vizuri kombe la Dunia ingawa hawajawahi kupita hatua ya robo fainali tangu wapoteze fainali mwaka 1990 kwa kufungwa na Ujerumani 1-0.
Mabao ya Argentina yalifungwa na Palacio dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza, Javier Mascherano dakika ya 51 na Rodriguez akagonga msumari wa mwisho dakika ya 64.
Italia kwa mara nyingine tena wamepata sare ya 1-1 wakiwa nyumbani dhidi ya Luxembourg. Vijana wa Prandeli walikuwa wa kwanza kupata goli dakika ya 9 kupitia kwa Marcishio kabla ya wageni Luxembourg kusawazisha dakika ya 85 kupitia kwa Chanot.
Waingereza walipata droo pia lakini wao wakiwa wamesafiri hadi Ecuador ambako walicheza na timu ya taifa hilo.Wenyeji Ecuador walikuwa wa kwanza kuliona lango la Uingereza kupitia mshambuliaji wao Enner Valencia.
Uingereza walipumua kupitia kwa Wayne Rooney dakika ya 29 baada ya kufunga goli la kusawazisha. Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa matokeo ya 1-1, kipindi cha pili Uingereza walipata goli la kuongoza dakika ya 51 kupitia kwa Rickie Lambart kabla ya wenyeji kusawazisha dakika ya 70 kupitia kwa Michael Arroyo na matokeo kuwa 2-2.
Uholanzi wameshinda mechi yao ya kirafiki dhidi ya Wales kwa magoli mawili ya Arjen Robben na Jeremain Lens.