Serikali ya Jamhuri ya Dominican imempiga marufuku Miley Cyrus kufanya onesho lake katika mji mkuu kutokana na uchezaji wake.
Msanii huyo alikuwa afanye onesho lake Septemba 13 jijini Santo Domingo.
Mamlaka zinasema zimezuia onesho hilo kwa sababu msanii huyo “hucheza miondoko ambayo ni kinyume na mila na desturi, na ambayo ni kosa kwa sheria za Dominican”.
Tiketi kuanzia dola 27 hadi dola 370 zimekuwa zikiuzwa kuanzia mwezi Julai.
Tume ya serikali ya Jamhuri ya Dominican inayosimamia maonesho ya hadhara imewahi kupiga marufuku uchezaji wa nyimbo katika redio ambazo ilidhani zinakiuka maadili.
Hakuna yeyote kati ya Cyrus au waandalizi waliosema chochote kuhusiana na kufutwa kwa onesho hilo.
Msanii huyo anatarajiwa kuhudhuria tuzo za MTV za video bora – MTV Video Music Awards zitakazofanyika kesho Jumapili- ingawa hatofanya onesho lolote.
Katika tuzo za mwaka jana alikonga vichwa vya habari baada ya kucheza miondoko ya kutatanisha na mwimbaji Robin Thiket.