Na Waandishi Wetu
KLABU ya mastaa wa filamu
jijini Dar es Salaam, Bongo Movie ‘Bongo Muvi’ imepasuka katikati kisa
kikidaiwa kuwa ni lile tamko linalodaiwa kutolewa na mwenyekiti wa klabu
hiyo, Vincent Honorati Lasasi Kigosi ‘Ray’ kuwa mwanachama yeyote wa
kundi hilio asitie miguu kwenye msiba wa baba mzazi wa mwenzao, Wema
Sepetu, marehemu Balozi Isaac Sepetu.
Tukio hilo la katazo lilitokea wakati wa maombolezo ya kifo cha
mzee Sepetu kilichotokea Oktoba 27, mwaka huu katika Hospitali ya TMJ
kwa ugonjwa wa kisukari ambapo msiba ulikuwa nyumbani kwake, Sinza Mori
jijini Dar es Salaam.
LAWAMA ZOTE KWA RAY
Kufuatia madai hayo, baadhi
ya wasanii wa Bongo Muvi (majina tunayo) wamekuwa wakitoa lawama zao kwa
Ray huku wengine wakidai wamejitoa kwenye kundi hilo kwa sababu halina
umoja na limejaa unafiki.
Maneno hayo yalianza kusambaa baada ya Wema kumaliza kumzika baba yake Oktoba 31, mwaka huu mjini Zanzibar.
RAY AAGIZWA AITISHE KIKAO CHA DHARURA KUMJADILI
Habari za uhakika zinasema kwamba, wasanii waliotangaza kujiengua
klabuni humo wameshamuomba Ray aitishe kikao cha dharura kwa ajili ya
kuzungumzia hatua yake ya kuwapiga marufuku wasanii hao kutoshiriki
msiba wa mzee Sepetu huku akijua wema wa binadamu unapatikana kwenye
kushiriki mazishi ya wenzake.
“Kikubwa zaidi ni kwamba, Ray wakati akisambaza zile meseji alisahau
kuwa kuna siku Wema aliwahi kuwaalika wasanii wa Bongo Muvi nyumbani
kwake Makumbusho (Dar) wakala na kunywa, mbona hawakugoma kwenda?”
alihoji staa mmoja aliyepinga katazo la Ray.
NJAMA ZA KUINGAMIZA KABISA BONGO MUVI ZAUNDWA CHINI KWA CHINI
Habari zaidi kutoka kwenye kundi linalodaiwa kujimega kwenye mpasuko
huo zinasema kuwa kuna njama za makusudi za kuiangamiza klabu hiyo kwa
kuwa mbali na mwenyekiti huyo kuwazuia wajumbe wasiende msibani kwa mzee
Sepetu lakini imekuwa ikiendeshwa kitemi na kibaguzi.
Ilisemakana kuwa kuna wasanii wameifanya klabu hiyo kama yao huku
wengine wakiwa hawatakiwi hata kukohoa jambo walilosema si sawasawa.
“Kwa mpasuko huu, wasanii waliochukizwa na Ray wamesema nao wao
wanakazia hapahapa, Bongo Muvi lazima iangamie moja kwa moja, isiwepo
tena,” alisema msanii mmoja ambaye jina lake linapanda kwa kasi.
KISINGIZIO CHA WASANII WANAFIKI CHAPINGWA
Maumivu makali zaidi yaliibuka kufuatia baadhi ya wasanii waliotaka
kujifanya hawajapata meseji ya Ray ambapo walisema walishindwa kushiriki
msiba huo kwa sababu walikuwa ‘shooting’.
“Kuna wasanii walishindwa
kuweka wazi kwamba walipokea meseji ya katazo ya Ray, walipopigiwa simu
na wenzao kuulizwa kwa nini hawaonekani msibani kwa Wema walisingizia
eti wako location wanarekodi!
“Kwa akili za kawaida, mwenzenu kafiwa
mnaweza kushikwa na ubize wa kurekodi filamu? Hawa ni wanafiki,
walisingizia vile ili ionekane wana hudhuru,” alisema staa mwingine.
MAMA WEMA ASHTUSHWA
Akizungumza na waandishi
wetu kwa mara ya kwanza baada ya kusikia mwanaye alisusiwa msiba wa baba
yake, mama mzazi wa Wema, Mariam Sepetu alionesha kusikitishwa sana na
kitendo hicho.
Alisema kitendo hicho kilitokea wakati ambao Wema au
familia nzima ilikuwa inasaka faraja na si mfarakano kwa vile kufiwa
kupo na hakuna dalili wala kujiandaa.
“Nilisikitika sana, lakini
siwezi kusema mengi kwa sababu vijana wanataka mwongozo ili kwenda
mbele, naamini watakaa na kuondoa tofauti zao,” alisema mama huyo mwenye
mapenzi makubwa na mastaa wa filamu Bongo.
KATAZO LA RAY
LILISIMAMIA HIVI
Habari
kutoka chanzo chetu makini zilidai kuwa hoja dhaifu iliyotumiwa na Ray
ni kwamba Wema huwa haendi kwenye misiba ya wenzake hivyo walitaka na
yeye amzike baba yake mwenyewe.
MISIBA ILIYOTOLEWA MFANO
Ulitolewa mfano msiba wa aliyekuwa staa
wa filamu za Bongo, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ aliyefariki dunia Januari 2,
mwaka huu ambapo Wema alishindwa kufika kwa sababu alikuwa studio
akirekodi wimbo wake mpya ambao haujatoka hadi leo.
MISIBA ALIYOSHIRIKI
Ilidaiwa kuwa Wema huwa hashiriki misiba ya
wenzake, ikatolewa mifano misiba miwili aliyoshriki kuwa ni marehemu
Sharo Milionea (Hussein Mkiety) na (Steven) Kanumba kwa sababu alikuwa
mtu wake.
ANACHOSIMAMIA WEMA
Akizungumzia tukio la kususiwa msiba wa baba yake, Wema alifunguka:
“Nimesikitishwa na kitendo hicho naamini hakikuwa cha haki, mimi
nimekuwa nikihudhuria misibani kwa watu mbalimbali na si kweli kwamba
niko kivyangu, nimehukumiwa bure.”
RAY AINGIA ‘PANGONI’
Juzi Jumanne, Amani lilimsaka Ray kwa njia ya simu ili aelezee ukweli wa madai hayo lakini aliingia ‘pangoni’ (hakupokea simu).
Hata hivyo, katika gazeti ndugu la hili, Ijumaa la Ijumaa, Novemba
Mosi, 2013 ukurasa wa mbele ambapo kuna habari yenye kichwa; WEMA SEPETU
ASUSIWA MSIBA, Ray aliulizwa kuhusu madai hayo ambapo alijibu:
“Mh!
Kweli Wema haendagi kwenye misiba ya watu, hata mimi sikumuona kwa
Sajuki ingawa sijui kama alionekana baadaye ila kwa sasa niko sehemu
mbaya nitakupigia baadaye tuongee kwa kirefu.”
Hakupiga.
MASTAA KIDUCHU MSIBANI
Pamoja na katazo hilo la
Ray, wasanii wengine waliamua kwenda msibani Sinza – Mori (Dar) na
wachache sana kwenye mazishi, Zanzibar.
Baadhi ya wasanii hao ni
pamoja na Kajala Masanja, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Mahsein Awadh ‘Dk.
Cheni’, Jacob Stephen ‘JB’, Yobnesh Yusuph ‘Batuli’, Salum Mchoma
‘Chiki’, Ahmed Olotu ‘Mzee Chilo’ na Jacqueline Wolper.
WASIOFIKA MSIBANI
Wengi walimsusia msiba Wema,
lakini majina makubwa zaidi wakiongozwa na Ray mwenyewe ni Single
Mtambalike ‘Richie’, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’, Irene Paul,
Blandina Chagula ‘Johari’, Ndumbangwe Misayo ‘Thea’ na Ruth Suka
‘Mainda’
CHANZO;GPL.